Mji huu wa kihistoria umepata utakatifu na nafasi yake ya kidini kutokana na uwepo wa haram takatifu ya Amirul Muuminin (Amani iwe juu yake); nembo muhimu zaidi ya mji huu, moyo wa Najaf, na kimbilio la nyoyo zenye shauku ambazo kila mwaka huwaita mamilioni ya wafanyaziara kutoka kote ulimwenguni.
Hata hivyo, harakati ya kielimu huko Najaf inaweza kuchukuliwa kama mwendelezo wa njia ya shule ya Kufa; kwani kundi la wanachuoni wa Kishia na wanafunzi wa elimu, mwanzoni mwa karne ya nne Hijria, walihamia mji huu na kuufanya kuwa kituo cha Marja’ ya kidini. Baada ya hapo, hususan katika kipindi cha Al-Buwayh, familia nyingi za kielimu zilielekea Najaf na kwa msaada wa utawala huo, mji huu ulishamiri kwa kasi katika nyanja za ujenzi na maendeleo pamoja na nyanja za kielimu na kitamaduni.
Wakubwa wa Kwanza wa Kielimu Waliokaa Najaf
Mnamo mwaka 296 Hijria, “Hussein bin Ahmad”, maarufu kama “Al-Mastur” au “Al-Maktum”, alielekea Najaf Ashraf kuzuru haram takatifu ya Amirul Muuminin Ali (Amani iwe juu yake) na katika safari hiyo alianzisha mawasiliano na idadi ya wanachuoni na shakhsia mashuhuri wa kielimu, akiwemo “Abu al-Qasim Hussein bin Ruh” na “Ali bin Fadhl”.
Muda mfupi baadaye, mnamo mwaka 308 Hijria, “Sayyid Sharifuddin Muhammad”, maarufu kama “Ibn al-Sidrah”, alifika Najaf. Alifikia cheo cha Naqib wa wanachuoni na akabaki katika mji huu hadi mwisho wa umri wake, na familia yake ikajulikana kama “Bani al-Sidrah”.
“Sheikh Ahmad bin Ali al-Najashi” katika kitabu chake cha Rijal anaandika kuwa alimuona “Is-haq bin Hasan bin Bakran al-Uqra’i al-Tammar” huko Kufa na akapokea kitabu cha Kulayni kutoka kwake. Sheikh Agha Bozorg Tehrani akifafanua anaongeza kuwa neno “Mujawir” linamaanisha ukazi wa kudumu katika maeneo matakatifu, jambo linaloonyesha kuwa yeye alikuwa mkazi wa Najaf na si mfanyaziara tu.
Pia, Sheikh al-Najashi mnamo mwaka 400 Hijria alisafiri kuelekea Najaf na huko alikutana na kundi la wanachuoni, akiwemo “Sheikh Abu Nasr Hebatullah bin Ahmad bin Muhammad (Ibn Barina)” na mwalimu wake “Abu Abdullah bin Khamri”, na kufanya nao mazungumzo.
Kushamiri na Ukuaji wa Kielimu wa Mji wa Najaf
Baada ya kushamiri kwa kielimu kwa Najaf mwishoni mwa karne ya nne Hijria, kitovu kikuu cha elimu na malezi katika mji huu kilikuwa ni uwanja (Sahn) wa haram ya Alawi; mahali ambapo palikuwa pakiwahifadhi wanafunzi wa elimu na fadhila. Mtume Mtukufu (Rehema na Amani ziwe juu yake na aali zake) alikuwa amesema kuhusiana na jua linalong’aa la mji wa Najaf, Amirul Muuminin (Amani iwe juu yake): “Mimi ni mji wa elimu na Ali ni mlango wake. Basi yeyote anayetaka elimu, lazima aingilie mlangoni.”
Harakati ya kielimu huko Najaf Ashraf ilipata kasi ya kustaajabisha kutokana na kuhama kwa “Sheikh al-Taifa Abu Ja’far Muhammad bin Hasan al-Tusi” kutoka Baghdad kwenda najaf mnamo mwaka 448 Hijria. Alipanga mfumo wa elimu wa Hawza ya Najaf na kuandika vitabu vingi katika fiqhi, tafsiri, hadithi, kalamu (theolojia), na rijal, na hivyo akashika nafasi ya uongozi wa kidini wa Shia. Baada ya kufariki kwake mwaka 460 Hijria, Najaf iligeuka kuwa moja ya vituo vikubwa vya kielimu na kishule vya Shia Imamiya, na wanafunzi kutoka kote katika ardhi za Kiislamu walikuwa wakielekea mji huu kwa ajili ya masomo.
Marja’ wa kidini na wanachuoni wakubwa walianzisha shule (madrasa) nyingi katika mitaa ya kale ya Najaf, hususan katika Sahn ya Alawi na Madrasa ya Gharawi. Kutoka katika shule hizi, maelfu ya wanasayansi, mujtahidina, na wafikiriaji mashuhuri walitokea ambao walikuwa na mchango mkubwa katika kushamiri kwa kielimu na kitamaduni kwa mji huo. Mbali na shughuli za kidini, Najaf ilikuwa ni uwanja wa wahifadhi wa vitabu, washairi, waandishi, na wahubiri; uwepo ambao uliongeza utajiri wa kielimu na kitamaduni wa mji huo.
Maktaba; Hazina Tajiri na Zenye Thamani za Najaf
Najaf ilipata umaarufu mkubwa hususan kutokana na mazingira yake tajiri ya kielimu na uwepo wa hazina na maktaba nyingi zilizosheheni hati za kale (manuscripts) adimu na kazi zenye thamani. Maktaba hizi na vitabu hivyo vilikuwa vikipatikana kwa wanachuoni, wataalamu wa fasihi, na watu wa utamaduni, na miongoni mwa hizo, maktaba ya “Rawdha al-Haydariyyah” ilikuwa na nafasi ya pekee. Mikusanyiko kama hiyo ilikuwa ni dhihirisho la wazi la umuhimu wa kielimu na kistaarabu wa Najaf miongoni mwa vituo vya Kiislamu.
Mbali na hayo, kushamiri kwa soko la vitabu na harakati za kifikra huko Najaf Ashraf kulifungua njia kwa uanzishwaji wa mitambo ya uchapishaji na majarida mengi mwanzoni mwa karne ya kumi na nne Hijria. Jarida la kwanza la Kiarabu nchini Iraq lililoitwa “Al-Ilm” chini ya mhariri “Allamah Muhammad Ali Hebatuddin al-Shahrastani”, lilichapishwa mnamo mwaka 1328 Hijria.
Najaf, daima katika kipindi chote cha historia, imekuwa kituo cha kueneza elimu na fikra za Kiislamu na chimbuko la Marja’ ya Shia; mji ambao kwa takriban milenia moja, umebeba jukumu la uongozi wa kidini na kielimu. Mji huu unaendelea kuwa shabaha ya wanafunzi na watafiti kutoka kote ulimwenguni, na kila mwaka makumi ya wanachuoni na mujtahidina huhitimu hapo na kueneza utamaduni na maarifa ya Ahlul Bayt (Amani iwe juu yao) katika pembe zote za dunia.
Najaf Katika Zama za Kudhihiri
Si siri kuwa Maimamu maasumu (Amani iwe juu yao) walikuwa na mtazamo wa pekee kuelekea ardhi ya Iraq. Amirul Muuminin Ali (Amani iwe juu yake) alikuwa akijua nafasi ya juu na umuhimu wa mji wa Najaf; kwa sababu hiyo, mnamo mwaka 36 Hijria aliuhamisha mji mkuu wa ukhalifa wa Kiislamu kutoka Madina Munawwara kwenda Kufa. Juhudi hizi ziliendelea katika zama za Maimamu wengine (Amani iwe juu yao) ili kuonyesha kuwa Iraq, iwe kijiografia au kijamii na kitamaduni, ina nafasi ya pekee na ya kipekee katika mpango wa kimungu; mpango ambao kulingana nao, ardhi hii yenye baraka itakuwa ndiyo kituo cha kuanzia harakati ya Imam Mahdi (Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake) kwa ajili ya kuwakomboa wanadamu dhidi ya dhuluma na ukandamizaji na kuanzisha serikali ya haki na uadilifu wa kimungu.
Riwaya za ghaibu za Ahlul Bayt (Amani iwe juu yao) pamoja na ushahidi mbalimbali wa kihistoria na kiroho, zinaeleza wazi kuwa Iraq katika zama za kudhihiri itakuwa chimbuko na kituo kikuu cha mpango wa Ahlul Bayt (Amani iwe juu yao), na si ardhi nyingine yoyote. Katika kipindi hicho, Imam Mahdi (Amani iwe juu yake) ataifanya Kufa ya Alawi kuwa mji mkuu wa serikali yake iliyoahidiwa. Na kwa namna hiyo, kutokea Najaf Ashraf akiwa na watu wanaostahili na wafuasi waaminifu, bendera ya Uislamu asilia wa Muhammad (Rehema na Amani ziwe juu yake na aali zake) itapandishwa na kusambaa kote ulimwenguni.
“Sheikh Muhammad bin Ibrahim al-Nu’mani” kwa sanadi yake kutoka kwa Abu Hamza al-Thumali anapokea kuwa Imam Muhammad Baqir (Amani iwe juu yake) alisema:
“Ewe Thabit! Kama ninamuona Al-Qaim wa Ahlul Bayt wangu akidhihiri kwenye muinuko wa Najaf yenu na akaashiria kuelekea Kufa. Atakapodhihiri Najaf, atapandisha bendera ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (Rehema na Amani ziwe juu yake na aali zake). Kwa kupandishwa kwa bendera hiyo, malaika wa Badr watamshukia…”
Imam Hasan al-Askari (Amani iwe juu yake) naye alisema kuhusu kughibu kwa mwanawe Imam Mahdi (Amani iwe juu yake):
“Yeye ana kughibu ambako wajinga watatangatanga humo, wafuata batili wataangamia, na wale wanaoweka wakati wa kudhihiri watakuwa waongo. Kisha atadhihiri, na kama ninaona bendera nyeupe zikipepea juu ya kichwa chake huko Najaf ya Kufa.”
Amirul Muuminin (Amani iwe juu yake) katika kumuelezea Al-Qaim (Amani iwe juu yake) alisema:
“Kama ninamuona akitokea Wadi al-Salam kuelekea Msikiti wa Sahla, akiwa juu ya farasi mweupe mwenye alama kwenye paji la uso na miguuni, huku akiwa na utukufu na akiomba dua akisema: La ilaha illa Allah, haqqan wa yaqinan…“
Katika riwaya ya kuvutia imeelezwa kuwa Mufaddal bin Umar siku moja alimuuliza Imam Ja’far Sadiq (Amani iwe juu yake):
“Ewe Imam wa haki, nyumba ya Mahdi na mahali pa mkusanyiko wa waumini patakuwa wapi? Imam akajibu: Mji wa ufalme wake ni Kufa; mahali pake pa kutoa hukumu ni Msikiti Mkuu wa Kufa, hazina yake na mahali pa kugawa ghanima ni Msikiti wa Sahla, na mahali pake pa faragha patakuwa ni vilima vyeupe vya Najaf.”
Mufaddal akauliza tena: “Je, waumini wote watakuwa Kufa?”
Imam akajibu: “Ndiyo, naapa kwa Mwenyezi Mungu hakuna muumini atakayebaki isipokuwa atakuwa Kufa au pembezoni mwake. Thamani ya ardhi itapanda sana kiasi kwamba eneo dogo litauzwa kwa bei kubwa sana. Ukubwa wa Kufa utafika maili 54 na majumba yake yatafika hadi Karbala. Mwenyezi Mungu ataifanya Karbala kuwa kituo na kimbilio ambalo malaika na waumini watakuwa wakipishana humo. Karbala itapangiwa nafasi ya juu na baraka kuu; kiasi kwamba ikiwa muumini atasimama hapo na kuomba haja kwa Mungu, Mwenyezi Mungu atampa mara elfu moja zaidi ya milki ya dunia.”
Vyanzo:
Imetolewa katika kitabu “Tarikh al-Marqad al-Alawi al-Mutahhar” (Historia ya Haram Takatifu ya Alawi)