Katika maandiko ya kihistoria, majina tofauti yametajwa kwa ajili ya Najaf, yakiwemo Ghari au Gharian na Mashhad, ambayo kila moja hubeba maana maalum.
Maana ya Neno “Najaf”
Katika lugha ya Kiarabu, neno “Najaf” kitaalamu hutumika kumaanisha eneo lililoinuka ambapo maji hayatuami juu yake.
Vyanzo mbalimbali vinaeleza hivi:
- Al-Jawhari amesema: “Najaf na Najafah ni eneo refu lenye umbo la mstatili ambapo maji hayakusanyiki.”
- Al-Bakri na Al-Zamakhshari wamebainisha: “Najaf ina maana ya kimo na ardhi kavu na ngumu, na imepewa jina hilo kwa sababu hiyo.”
- Al-Azhari amesema: “Najafah ni eneo lililopo nje ya Kufa ambalo huzuia maji ya mafuriko kupanda.”
- Ibn Qutaybah al-Dinawari amesema: “Ardhi kando ya mto Furati (Euphrates) na nyuma yake zilijulikana kama Maltat na Najaf kwa mfuatano huo.”
Kwa ujumla, neno “Najaf” hufafanuliwa kama muinuko kutoka ardhini na eneo ambalo maji hayatuami.
Sababu ya Kuupa Mji Jina la “Najaf”
Dkt. Mustafa Jawad anasema:
“Jina la Najaf linatokana na sifa zake za kijiografia; ni ardhi iliyoinuka inayofanya kazi kama kizingiti, ikizuia maji kuingia na kuyaweka mbali. Yaani, ardhi ya Najaf hubaki kavu hata wakati wa mafuriko.”
Mwanahistoria Muhammad Hussein Hirz al-Din naye anaeleza:
“Jina la Najaf linaweza kutokana na nafasi yake ya pekee ya kijiografia kati ya tambarare ya mashapo na nyanda za juu za jangwa, sawa na kizingiti cha mlango kinachotenganisha maeneo mawili. Kwa sababu hiyo, umeitwa ‘Kizingiti cha Jangwa la Iraq’ na kimo chake kimefanya jina hilo kuwa kitambulisho cha eneo hili. Nafasi hii pia iliifanya Najaf kuwa mahali pazuri kwa mapumziko ya misafara na wasafiri wanaoingia Iraq.”
Majina Mengine ya Mji wa Najaf
Eneo la Najaf katika historia limejulikana kwa majina mengi. Mashuhuri zaidi ni “Najaf, Ghari, na Mashhad”. Pia majina kama “Khadd al-Adhra, Dhahr, Rabwah, Toor Sina, Judi, Lisan, Dhakuwat al-Bidh, Wadi al-Salam, Thawiyya, na Baniqya” yametajwa.
Jina “Najaf” limekuwa likitumika tangu kale na limetajwa katika hadithi za Ahlul Bayt (Amani iwe juu yao). Kulingana na riwaya kutoka kwa Imam Sadiq (Amani iwe juu yake):
“Najaf mwanzoni ulikuwa mlima mkubwa ambao wakati wa gharika ya Nuhu (Amani iwe juu yake) ulisambaratika kwa amri ya Mwenyezi Mungu na kugeuka kuwa bahari, kisha ardhi kavu. Tangu wakati huo, uliitwa Nay-Jaff yaani ‘imekauka’, na baadaye ikawa rahisi kuitwa Najaf.”
Mji wa Najaf Ulijulikana kwa Jina Gani?
Hapo zamani, Najaf kutokana na hali ya hewa ya wastani, hewa safi, ardhi yenye rutuba na kuchomoza kwa maua na mimea (hasa wakati wa machipuko), uligeuka kuwa eneo la mapumziko na burudani kwa wafalme, makhalifa na wakubwa.
Majumba ya kifalme, kuta, na makanisa ya kale yalijengwa pembezoni mwake, na eneo hili lilijulikana kwa kuwa na ardhi safi na yenye harufu nzuri. Kutokana na uzuri wa asili yake, Waarabu wa zama za kijahili waliuita “Khadd al-Adhra” au “Khadd al-Adhari” (shavu la mwanamwali).
Maana ya Majina Mengine ya Najaf
1. Neno “Ghari”
Ghari ni moja ya majina maalum ya Najaf. Neno hili katika lugha ya Kiarabu lina maana ya “kitu kizuri na chema” na wakati mwingine humaanisha “kitu kilichopambwa na kupakwa rangi”.
“Gharian” ilitumiwa kumaanisha majengo mawili marefu (kama minara miwili) huko Najaf. Majengo haya yalikuwa nje ya mji wa Kufa na karibu na haram ya Amirul Muuminin (Amani iwe juu yake), yakitumika kama alama ya kihistoria.
2. Neno “Mashhad”
Jina lingine la Najaf ni Mashhad. Jina hili lilishika kasi baada ya kufichuliwa kwa kaburi takatifu la Amirul Muuminin (Amani iwe juu yake) na lina maana ya mahali pa mkusanyiko wa watu au dharih.
Imam Sadiq (Amani iwe juu yake) katika ziyara yake ya kwanza Najaf, alimwambia Safwan Jammal: “Hapa ndipo Mashhad ya Amirul Muuminin (Amani iwe juu yake)”.
Wasafiri mbalimbali wamerejelea jina hili:
- Al-Harawi aliuita “Mashhad ya Amirul Muuminin”.
- Ibn Battuta alitaja “Mji wa Mashhad ya Ali bin Abi Talib huko Najaf”.
Kadiri mji ulivyopanuka kuzunguka haram, jina Mashhad halikutumika kwa dharih pekee bali kwa mji mzima. Kutokana na hili, wakazi wake waliitwa “Mashahidah” na asili yao ikawa “Mash-hadi”.
Chanzo:
Imetolewa katika kitabu “Tarikh al-Marqad al-Alawi al-Mutahhar” (Historia ya Haram Takatifu ya Alawi)