Most searched:

Tukio la Ashura katika Utabiri wa Amirul Muuminiin (amani iwe juu yake)

Miaka mingi kabla ya tukio la Ashura, machozi ya Mtume (rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na Aali zake) na Amirul Muuminiin (amani iwe juu yake) yalikuwa yakisimulia hatima ya Karbala. Bwana wa Wachamungu, kwa elimu ya ghaibu, aliinusa ardhi ya eneo hili na kutambua sehemu ambazo wanaume watakaouawa shahidi humo wangekuwa. Riwaya hizi zinasimulia shahada ya Imam Hussein (amani iwe juu yake) kwa mtazamo wenye nuru na kupitia utabiri wa Amirul Muuminiin (amani iwe juu yake).

Miongoni mwa matukio yote makubwa katika historia ya Uislamu, hakuna tukio lililofungamana kwa kiwango kikubwa na utabiri wa Mtume wa Mwisho (rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na Aali zake) na Amirul Muuminiin (amani iwe juu yake) kama shahada ya Imam Hussein (amani iwe juu yake). Bwana wa Wachamungu, sambamba na kutabiri shahada ya Imam Hussein (amani iwe juu yake), alitaja pia baadhi ya maelezo ya tukio la Ashura, kama vile eneo la mahema, mahali pa kuuwawa, mahali pa kuzikwa, kutopata msaada kwa Imam Hussein (amani iwe juu yake), na hata matukio yaliyofuata baada ya Ashura. Utabiri huu haukuwa tu taarifa kuhusu tukio moja, bali ulikuwa onyo la Kiungu kwa ajili ya kuamsha dhamiri na kubainisha njia ya haki na batili.

Habari ya Kuhuzunisha ya Karbala

Amirul Muuminiin (amani iwe juu yake), kwa utabiri wake na kwa kukumbusha simulizi ya turba ya Karbala, alidhihirisha uhusiano wa kina kati ya msiba wa Imam Hussein (amani iwe juu yake) na ujumbe wa Kiungu katika njia ya kuelekea Swiffin.

Abdullah bin Yahya, ambaye alikuwa miongoni mwa wapokezi wa riwaya na askari wa Amirul Muuminiin (amani iwe juu yake), anasimulia:

“Tulikuwa pamoja na Amirul Muuminiin Ali bin Abi Talib (amani iwe juu yake) tukielekea Swiffin. Imam alipofika sehemu iliyo mkabala na Nainawa, alisema: ‘Ewe Abdullah! Punguza mwendo.’

Kisha akaendelea:

‘Siku moja nilifika mbele ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na Aali zake), huku macho yake matukufu yakiwa yamejaa machozi. Nikasema: Baba na mama yangu wawe fidia kwako, ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Kwa nini macho yako matukufu yana machozi? Je, kuna mtu aliyekukasirisha?’

Mtume (rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na Aali zake) akasema:

‘Hapana; lakini Jibril alikuwa kwangu na amenijulisha kwamba Hussein wako atauwawa shahidi kando ya Furat.’

Kisha Jibril akasema:

‘Je, ungependa kuinusa turba ya Hussein (amani iwe juu yake)?’

Nikasema:

‘Ndiyo.’

Kisha akanyoosha mkono wake, akaleta konzi moja ya turba(udongo) ya Hussein (amani iwe juu yake) na kunipa. Sikuweza kujizuia kulia. Jina la ardhi hiyo ni Karbala.” [1]

Karbala; Mahali pa Kukutana Watu wa Peponi

Bwana wa Wachamungu, alipokuwa akipita Karbala, kwa machozi na basira alitangulia kueleza hatima ya shahada ya masahaba wa Imam Hussein (amani iwe juu yake).

Juwayriyya bin Mushir al-Abdi alikuwa miongoni mwa masahaba wa karibu, wa kuaminika na wapendwa wa Bwana wa Wachamungu. Alikuwa pamoja na Amirul Muuminiin (amani iwe juu yake) katika vita vya Swiffin na Nahrawan. Anasimulia kutoka kwake:

“Tulipoelekea Swiffin pamoja na Amirul Muuminiin (amani iwe juu yake) na kufika kwenye vilima vya Karbala, Amirul Muuminiin (amani iwe juu yake) alisimama upande mmoja wa jeshi, akatazama maeneo ya pembeni na kutoa machozi. Kisha akasema:

‘Naapa kwa Mwenyezi Mungu, hapa ndipo mahali pao pa kusimama na mahali pa kifo chao.’

Wakauliza:

‘Ewe Amirul Muuminiin (amani iwe juu yake), mahali hapa ni wapi?’

Akasema:

‘Hapa ni Karbala; mahali watakapouwawa wanaume ambao wataingia Peponi bila hisabu.’

Kisha akaendelea na safari. Siku hiyo watu hawakuelewa maana ya maneno ya Imam mpaka tukio la shahada ya Hussein bin Ali (amani iwe juu yake) na masahaba wake lilipotokea Karbala.” [2]

Mtu Aliyekimbia Karbala

Kwa mujibu wa riwaya na taarifa za kihistoria, Amirul Muuminiin (amani iwe juu yake), alipokuwa akipita katika ardhi ya Karbala, sambamba na kutabiri shahada ya Imam Hussein (amani iwe juu yake), alitaja baadhi ya maelezo ya tukio la Ashura.

Harthama bin Salim, mmoja wa masahaba wa Bwana wa Wachamungu, anasimulia:

“Katika moja ya vita tulikuwa pamoja na Ali bin Abi Talib (amani iwe juu yake). Tulipofika Karbala, Imam alisimamisha Swalah. Baada ya kutoa salamu ya Swalah, alichukua konzi ya udongo wa eneo hilo, akaunusa na kusema:

‘Hongera kwako, ewe udongo! Kutoka kwako watainuka watu ambao wataingia Peponi bila hisabu.’

Anaendelea kusema:

‘Niliporudi kutoka vitani, nilimsimulia mke wangu Jardaa, ambaye alikuwa miongoni mwa wapenzi na Mashia wa Amirul Muuminiin (amani iwe juu yake), tukio hilo. Kwa mshangao nikamuuliza: Anawezaje kuyajua mambo haya ya ghaibu?

Mke wangu akasema:

“Ewe mtu! Acha maneno haya! Amirul Muuminiin (amani iwe juu yake) hasemi chochote isipokuwa haki.”

Harthama anaongeza:

‘Miaka mingi baadaye, Ubaidullah bin Ziyad alipotuma jeshi kwenda kupigana na Hussein bin Ali (amani iwe juu yake) pamoja na masahaba wake, mimi pia nilikuwa miongoni mwa wapanda farasi wa jeshi hilo.

Tulipolifikia jeshi la Hussein (amani iwe juu yake) na masahaba wake, nikaitambua sehemu hiyo. Ilikuwa ndiyo sehemu ileile ambayo Amirul Muuminiin (amani iwe juu yake) alikuwa ametushusha, na ndiyo sehemu ileile ambayo alichukua udongo wake, akaunusa na kusema maneno hayo.

Nikajutia kuja kwangu. Kisha nikapanda farasi wangu na kuelekea kwa Hussein (amani iwe juu yake), nikamsalimia na nikamsimulia yale niliyokuwa nimeyasikia kutoka kwa baba yake kuhusu ardhi hii.’

Imam Hussein (amani iwe juu yake) akaniuliza:

‘Je, uko pamoja nasi au dhidi yetu?’

Nikasema:

‘Ewe mwana wa Mtume wa Mwenyezi Mungu! Siko pamoja nanyi wala dhidi yenu. Nimewaacha familia yangu, na ninaogopa Ibn Ziyad atawaathiri.’

Imam Hussein (amani iwe juu yake) akasema:

‘Basi kimbia na uende mbali, ili usishuhudie kuuwawa kwetu. Naapa kwa Yule ambaye roho ya Muhammad iko mkononi Mwake, yeyote atakayeona leo namna tunavyouawa na asitusaidie, Mwenyezi Mungu atamtupa Motoni.’

Harthama alisema:

‘Nami nikakimbia kutoka katika ardhi hiyo ili nisishuhudie shahada yao.’” [3]

Utabiri wa Bwana wa Wachamungu Kuhusu Tukio la Ashura

Amirul Muuminiin (amani iwe juu yake), kwa basira yake, alitabiri shahada na kudhulumiwa kwa Imam Hussein (amani iwe juu yake) nyuma ya Kufa na katika ardhi ya Karbala.

Harith al-A’war alikuwa miongoni mwa masahaba wa Amirul Muuminiin (amani iwe juu yake) na miongoni mwa watu wa kwanza walioweka kiapo cha uaminifu kwake Madina. Harith al-A’war, ambaye alikuwa akiandika Hadithi na hotuba za Amirul Muuminiin (amani iwe juu yake), anasimulia kwamba Imam alisema:

“Baba na mama yangu wawe fidia kwa Hussein, ambaye atauwawa shahidi nyuma ya Kufa! Naapa kwa Mwenyezi Mungu, ni kana kwamba ninawaona wanyama wa mwituni wakiweka shingo zao juu ya kaburi la Hussein na kumlilia na kumuomboleza kuanzia usiku hadi asubuhi. Wakati huo utakapofika, jihadharini na ukatili na dhuluma.” [4]

Pia Amirul Muuminiin Ali (amani iwe juu yake), alipokuwa akieleza mahali pa shahada ya Imam Hussein (amani iwe juu yake), alisema:

“Hussein (amani iwe juu yake) atauawa kwa namna ya ajabu. Ninaijua ardhi ambayo Hussein atauawa shahidi juu yake; ni ile ardhi iliyopo kati ya mito miwili.” [5]

Ushahidi wa Historia juu ya Utabiri wa Bwana wa Wachamungu

Katika tukio jingine, Amirul Muuminiin (amani iwe juu yake) alimkumbusha Baraa bin Azib, ambaye alikuwa miongoni mwa Masahaba wa Mtume (rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na Aali zake) na pia masahaba wake, kuhusu utabiri wa shahada ya Hussein wake mpendwa. Alimwambia:

“Mwanangu Hussein atauwawa; siku hiyo utakuwa hai, lakini hutamnusuru.”

Miaka ikapita na tukio la Karbala likatokea. Baada ya shahada ya Imam Hussein (amani iwe juu yake), Baraa bin Azib, ambaye kwa macho yake alishuhudia kutimia kwa maneno hayo, alikuwa akisema:

“Naapa kwa Mwenyezi Mungu, Ali bin Abi Talib (amani iwe juu yake) alisema kweli; kwa sababu Hussein aliuwawa nami sikumnusuru!”

Kisha akapatwa na majuto na masikitiko makubwa kwa kukosa kwake saada hiyo. [6]

Ewe Sababu ya Machozi ya Waumini Wote!

Amirul Muuminiin Ali (amani iwe juu yake), kwa mtazamo wake wenye basira, aliona katika uwepo wa Imam Hussein (amani iwe juu yake) chanzo cha machozi na huzuni za waumini.

Imam Ja’far Swadiq (amani iwe juu yake) anasema:

“Siku moja Amirul Muuminiin Ali (amani iwe juu yake) alimtazama mwanawe Imam Hussein (amani iwe juu yake) na kusema:

‘Ewe sababu ya machozi ya waumini wote!’

Imam Hussein (amani iwe juu yake) akauliza:

‘Baba yangu! Je, unamaanisha mimi?’

Amirul Muuminiin (amani iwe juu yake) akajibu:

‘Ndiyo, ewe mwanangu mpendwa.’” [7]

Vyanzo
[1] Bihar al-Anwar, Juzuu ya 44, ukurasa wa 247.
[2] Bihar al-Anwar, Juzuu ya 41, ukurasa wa 286.
[3] Waq’at Swiffin, Juzuu ya 1, ukurasa wa 140.
[4] Bihar al-Anwar, Juzuu ya 45, ukurasa wa 205.
[5] Bihar al-Anwar, Juzuu ya 44, ukurasa wa 262.
[6] Bihar al-Anwar, Juzuu ya 44, ukurasa wa 262.
[7] Bihar al-Anwar, Juzuu ya 44, ukurasa wa 280.

Yaliyomo zaidi

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *