Most searched:

Wilayah, Nguzo Muhimu ya Dini na Mafunzo ya Mungu katika Mtazamo wa Imamu Baqir (a.s)

Imamu Muhammad Baqir (a.s) anaitambulisha Wilayah si tu kama nguzo mojawapo ya dini, bali kama ufunguo wa kufahamu na kutekeleza ibada nyingine za Kiislamu na sharti la lazima kwa ajili ya kumjua Mola kwa kweli. Riwaya hizi, pamoja na kubainisha nafasi ya Amirul Muuminina (a.s) kama muhimili mkuu wa Wilayah, zinaonyesha wazi kwamba kukubali na kuwafuata Maimamu maasumu ni njia ambayo Mwenyezi Mungu ameichagua kwa ajili ya kuongoza wanadamu.

Tarehe na Mahali pa Kuuawa Shahidi Imamu Muhammad Baqir (a.s) kulingana na mapokezi maarufu, aliuawa shahidi mnamo tarehe saba Dhul-Hijjah mwaka 114 Hijiria. Inasemekana kuwa Mtukufu huyo aliuawa shahidi kwa sumu kwa amri ya Hisham bin Abdul-Malik (khalifa wa Ki bani umayya) na kupitia kwa Ibrahim bin Walid bin Abdul-Malik, gavana wa Madina. Kaburi lake takatifu linapatikana katika makaburi ya Baqi, kando ya baba yake Imamu Sajjad (a.s). Kipindi cha uimamu wa Imam Muhammad Baqir (a.s) kilianza mwaka 95 Hijiria – ambao ni mwaka aliofariki Imam Zaynul Abidin (a.s) – na kiliendelea hadi mwaka 114 Hijiria, yaani kwa muda wa miaka 19 na miezi kadhaa. [1]

Nafasi ya Wilayah katika Maneno ya Amirul Muuminina (a.s) na Ammar bin Yasir Imamu Baqir (a.s) ananukuu kwamba Amirul Muuminina Ali (a.s) alikuwa juu ya mimbari wakati mtu mmoja alipokuja kwake na kuomba idhini ya kusimulia riwaya aliyoisikia kutoka kwa Ammar bin Yasir, na ambayo Ammar aliinukuu kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w). Mtukufu huyo alisema: “Mcheni Mwenyezi Mungu na msizungumze kumhusu Ammar isipokuwa kile alichokisema yeye mwenyewe.” Amirul Muuminina (a.s) alikariri sentensi hii mara tatu na kisha akamwambia mtu huyo: “Sasa zungumza.” Mtu huyo alisema: “Nilimsikia Ammar akisema kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) alisema: Ninapigana kwa msingi wa Tanzil (dhahiri na matini) ya Qur’ani, na Amirul Muuminina (a.s) atapigana kwa msingi wa Ta’wil (batini na ufahamu wa kina) yake.” Amirul Muuminina (a.s) akasema: “Ninaapa kwa Mola wa Al-Kaaba, Ammar amesema ukweli. Neno hili, ni moja kati ya maneno elfu moja yenye maana nzito niliyojifunza kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w), na kila neno kati ya hayo, hunifungulia maelfu ya milango ya maarifa.” [2]

Matokeo ya Uadui Dhidi ya Wilayah Imamu Baqir (a.s) katika riwaya anaelezea nafasi ya juu ya Wilayah katika dini ya Uislamu. Alisema: “Adui wa Amirul Muuminina Ali (amani ie juu yake) haondoki duniani isipokuwa awe amekunywa fundo la maji yanayochemka ya Jehanamu.” Pia alisema: “Mtu anayepinga Wilayah ya Amirul Muuminina (a.s), kuswali na kufanya zinaa kwake ni sawa tu.” [3]

Maana ya Wakweli katika Qur’ani Kuna aya katika Qur’ani ambazo tafsiri zake za kina na zenye kuongoza za Maimamu maasumu, hufungua dirisha jipya kuelekea katika ufahamu wa haki. Imamu Baqir (a.s) amebainisha maana ya “wakweli” na mfano wake katika riwaya hii. Imamu Baqir (a.s) katika kutafsiri aya tukufu «یا أَیُّهَا الَّذینَ آمَنوا اتَّقُوا اللهَ وَ کونوا مَعَ الصّادِقینَ; Enyi mlioamini! Mcheni Mwenyezi Mungu na kuweni pamoja na wakweli – ‘Al-Tawbah’ 119» alisema: “Maana ya ‘wakweli’, ni Amirul Muuminina Ali bin Abi Talib (a.s); hivyo basi kuweni pamoja naye.” [4]

Imamu Mubin (Kiongozi Aliye Wazi) ni Nani? Katika riwaya kutoka kwa Imamu Baqir (a.s) anaelezea dhana na ishara ya Kiqur’ani ya “Imamu Mubin” kwa namna hii; alisema: “Aya hii ilipoteremshwa kwa Mtume (s.a.w.w): و کُلَّ شَيءٍ أحصَیناهُ في إمامٍ مُبینٍ; Na kila kitu tumekidhibiti katika kiongozi aliye wazi (Imamu Mubin) – ‘Yasin’ 12”, Abubakar na Umar walisimama na kuuliza: “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Je, maana ya ‘Imamu Mubin’, ni Taurati?” Mtume akasema: “Hapana.” Wakauliza tena: “Je, maana yake ni Injili?” Mtume akasema tena: “Hapana.” Kisha wakauliza: “Je, maana yake ni Qur’ani?” Mtume akajibu: “Hapana.” Wakati huo, Amirul Muuminina Ali (a.s) aliingia. Mtume (s.a.w.w) akasema: “‘Imamu Mubin’ ni huyu; yeye ni Imamu ambaye Mwenyezi Mungu mwenye baraka na utukufu, amekusanya elimu ya vitu vyote ndani yake.” [5]

Kumjua Mwenyezi Mungu; Kupitia Njia ya Wilayah ya Ahlul-Bayt Imamu Baqir (a.s) anaitambulisha njia ya kufikia kwenye uangalizi wa Kiungu na kuondosha pazia kati ya mja na Mwenyezi Mungu, kuwa ni kuwapenda Ahlul-Bayt. Kuhusiana na hili Abu Hamza al-Thumali ananukuu kwamba alimuuliza Imamu Baqir (a.s): “Kumjua Mwenyezi Mungu ni nini?” Mtukufu huyo akajibu: “Kumjua Mwenyezi Mungu, ni kumsadikisha Mwenyezi Mungu na Mtume Wake Muhammad (s.a.w.w) kuhusu Wilayah ya Amirul Muuminina Ali (a.s) na Maimamu baada yake, kuwafuata na kujiepusha na maadui zao.” [6]

Kumpenda Bwana wa Wachamungu ni Dhamana ya Kuwa Imara Katika Dini Imamu Baqir (a.s) kuhusu kumpenda Bwana wa Wachamungu na athari yake katika moyo wa muumini anasema: “Mwenyezi Mungu hakuweka mapenzi ya Amirul Muuminina Ali (a.s) katika moyo wa mtu yeyote, isipokuwa iwapo hatua yake moja itateleza (akafanya kosa), basi hatua yake nyingine (yakini na mapenzi yake) itabaki kuwa imara.” [7]

Tunda la Kuipenda Familia ya Muhammad (a.s) Imamu Baqir (a.s) kuhusu kuondosha pazia kati ya mtu na Mwenyezi Mungu na kufikia kwenye uangalizi wa Kiungu alisema: “Yeyote anayetamani pasiwepo na pazia kati yake na Mwenyezi Mungu ili amtazame Mwenyezi Mungu na Mwenyezi Mungu amwangalie, basi lazima aipende Familia ya Muhammad na ajiepushe na maadui zao na awe mfuasi wa Maimamu kutoka katika Familia ya Muhammad (a.s); anapokuwa hivyo, ataelekea kwa Mwenyezi Mungu na Mwenyezi Mungu pia atamwangalia yeye.” [8]

Kuletwa kwa Manabii; Kukiwa na Mhimili wa Wilayah na Kujiepusha na Maadui Imamu Baqir (a.s) kuhusu Wilayah ya Ahlul-Bayt na kujiepusha na maadui zao, na kupotea kwa mataifa alisema: “Mwenyezi Mungu hakumtuma nabii yeyote, isipokuwa ilikuwa pamoja na Wilayah yetu na kujiepusha na maadui zetu. Maana hii ipo pia katika aya ya 36 ya Surah An-Nahl ya Qur’ani:

وَلَقَدْ بَعَثْنَا فِي كُلِّ أُمَّةٍ رَسُولًا أَنْ اعْبُدُوا اللَّهَ وَاجْتَنِبُوا الطَّاغُوتَ ۖ فَمِنْهُمْ مَنْ هَدَى اللَّهُ وَمِنْهُمْ مَنْ حَقَّتْ عَلَيْهِ الضَّلَالَةُ

, Na wale waliopotea, ilikuwa kwa sababu ya kuikadhibisha Familia ya Muhammad (a.s).” [9]

Nguzo ya Tano ya Uislamu na Ufunguo wa Kukubaliwa kwa Matendo Zurarah ananukuu kutoka kwa Imamu Baqir (a.s) kwamba alieleza hivi kuhusu nguzo 5 za msingi za Uislamu na ile muhimu zaidi miongoni mwazo: “Uislamu umejengwa juu ya misingi mitano: Swala, Zaka, Funga, Hija na Wilayah.” Zurarah akauliza: “Ni ipi bora zaidi kati ya hizi?” Mtukufu huyo akasema: “Wilayah ni bora; kwa sababu Wilayah ni ufunguo wake, na kiongozi (Imamu) ndiye muongozaji wa kuyafikia.” Kisha akasema: “Fahamu! Iwapo mtu atapitisha usiku katika ibada, akafunga mchana, akatoa mali yake yote kama sadaka na akatumia umri wake wote kwenda Hija, lakini hamjui Kiongozi (Wali) wa Mwenyezi Mungu ili amfuate na kufanya matendo yake yote kwa mwongozo wake, hatakuwa na fungu lolote katika malipo ya Kiungu na hatahesabiwa miongoni mwa watu wa imani.” [10]

Chanzo
[1] Muntaha al-Aamal, Sheikh Abbas Qumi.
[2] Bihar al-Anwar, juzuu ya 32, ukurasa 299.
[3] Thawab al-A’mal wa ‘Iqab al-A’mal, juzuu ya 2, ukurasa 210; Bihar al-Anwar, juzuu ya 27, ukurasa 235.
[4] Al-Manaqib, juzuu ya 3, ukurasa 92.
[5] Tafsir Kanz al-Daqa’iq, juzuu ya 11, ukurasa 61.
[6] Tafsir al-Ayyashi, juzuu ya 2, ukurasa 116; Bihar al-Anwar, juzuu ya 27, ukurasa 57.
[7] Bihar al-Anwar, juzuu ya 65, ukurasa 199.
[8] Bihar al-Anwar, juzuu ya 27, ukurasa 51.
[9] Tafsir al-Burhan, juzuu ya 3, ukurasa 419.
[10] Ithbat al-Hudat, juzuu ya 1, ukurasa 117.

Yaliyomo zaidi

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *