Kituo cha «Qanbar» cha wahudumu wa Ataba tukufu ya Alawi kimeanza kampeni ya «Baba Yetu Ali» kwa agizo la moja kwa moja la msimamizi wa Ataba. Kampeni hii inalenga kukarabati na kutengeneza madawati ya shule katika maeneo yenye uhaba wa huduma mjini Najaf Ashraf.
Ahmad al-Zurqaani, mkuu wa Kituo cha «Qanbar» cha wahudumu wa Haram Tukufu ya Imam Ali, alisema katika mahojiano na Kituo cha Habari: «Wafanyakazi wa kituo chetu wameanza kazi katika wiki ya kwanza ya kampeni ya “Baba Yetu Ali”, kwa kushirikiana na taasisi za kujitolea. Kampeni hii inalenga kukarabati na kutengeneza madawati ya shule katika baadhi ya maeneo ya Najaf Ashraf. Inahusisha shule za vijijini, maeneo ya mbali na katikati ya mji, kwa kufuata ratiba maalumu.»
Swafaa al-Kilaabi, anayesimamia utekelezaji wa kampeni hii, pia alisisitiza: «Vifaa na mahitaji yote ya kampeni hii vimeandaliwa. Baada ya uratibu pamoja na Idara ya Elimu ya Mkoa wa Najaf Ashraf, vifaa hivyo vimegawiwa kwa zaidi ya vikundi 14 vya kujitolea ili vianze kazi za ukarabati na utengenezaji.»
Kampeni hii inatekelezwa kwa mwaka wa sita mfululizo katika juhudi za Ataba tukufu ya Imam Ali za kusaidia na kulea sekta ya elimu kwa uangalizi wa kibaba. Hatua hii inalenga kusaidia na kuimarisha miundombinu ya shule na kuandaa mazingira yanayofaa kwa wanafunzi.








