Maisha ya Imam Hassan (amani iwe juu yake) yaliambatana na majukumu mazito ya Uimamu na urithi wa baba yake mtukufu. Katika maisha ya Maimamu hawa wawili watukufu, kuna mshikamano wa kina katika fikra, utetezi wa haki na imani za kidini. Tangu alipozungusha upanga wa uadilifu akiwa kando ya baba yake katikati ya vumbi la Vita vya Jamal, hadi asubuhi ya shahada ya baba yake alipobainisha kutoka kwenye mimbari ya ‘Kufa’ iraq nafasi ya juu ya “Amirul Muuminiin” kwa Umma, ushirikiano huu haukuwa tu mwendelezo wa ujumbe, bali pia ulidhihirisha lengo la watukufu hao katika njia ya kuutukuza dini ya Mwenyezi Mungu.
Namna ya Shahada
Imam Hassan Al-Mujtaba (amani iwe juu yake) aliwekewa sumu na kuuwawa shahidi tarehe saba ya mwezi wa Swafar mwaka 50 Hijria, kwa njama ya Muawiya kupitia mke wake, Ja’da. Vikwazo vya Bani Umayya viliendelea hata baada ya shahada yake. Walizuia kuzikwa kwake karibu na Mtume (rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na Aali zake) ambao ulikuwa nsio wasiya wake , hivyo mwili wake mtukufu ukazikwa Baqi.
Majukumu ya Imam Hassan (amani iwe juu yake)
Baada ya shahada ya Amirul Muuminiin (amani iwe juu yake), Imam Hassan (amani iwe juu yake), akiwa mrithi na wasii wa baba yake, alichukua jukumu la kusimamia familia, wafuasi, mali za wakfu na shughuli zake za kutoa misaada. [1]
Kusifiwa na Baba yake
Amirul Muuminiin (amani iwe juu yake) alimwomba mwanawe, Imam Hassan (amani iwe juu yake), awahutubie watu, na baada ya hapo akamkirimu mwanawe.
Abu al-Jarud, aliyekuwa miongoni mwa wafasiri mashuhuri na masahaba wa Imam Baqir (amani iwe juu yake) na Imam Swadiq (amani iwe juu yake), anasimulia kwamba alimsikia Imam Baqir (amani iwe juu yake) akisema:
“Amirul Muuminiin (amani iwe juu yake) alimwambia Imam Hassan (amani iwe juu yake): ‘Leo simama na uwahutubie watu.’”
Imam Hassan (amani iwe juu yake) akasimama, akamhimidi Mwenyezi Mungu na akamswalia Mtume (rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na Aali zake). Kisha, kwa ilhamu ya Mwenyezi Mungu, akasema:
“Amirul Muuminiin (amani iwe juu yake) ana nafasi na daraja ambalo yeyote anayeingia humo huwa salama, na yeyote anayelipa mgongo huwa kafiri. Hayo ndiyo ninayosema, na ninamuomba Mwenyezi Mungu msamaha kwa ajili yangu na yenu.”
Baada ya Imam Hassan (amani iwe juu yake) kushuka kutoka kwenye mimbari, Amirul Muuminiin (amani iwe juu yake) alisimama, akambusu mwanawe kichwani na kusema:
“Baba yangu na mama yangu wawe fidia kwako.”
Kisha akasoma aya hii:
«ذُرِّيَّةً بَعضُها مِن بَعضٍ وَ اللهُ سَميعٌ عَليمٌ»
“kizazi kimoja kutokana na kingine na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua.” [2]
Ushujaa katika Medani ya Vita vya Jamal
Ushujaa wa Imam Hassan Al-Mujtaba (amani iwe juu yake) katikati ya moto wa Vita vya Jamal ulidhihirisha ukamilifu wa baba yake mtukufu ndani yake na kuthibitisha mwendelezo wa njia ya Uimamu.
Katika siku ya Vita vya Jamal, Amirul Muuminiin (amani iwe juu yake) alimpa mwanawe Muhammad bin Hanafiyya mkuki wake na kusema:
“Shambulia ngamia wa Aisha kwa mkuki huu.”
Muhammad akasonga mbele, lakini watu wa kabila la Bani Dhabba wakamzuia na hawakumruhusu kukaribia ngamia hawo. Aliporudi kwa baba yake, Imam Hassan (amani iwe juu yake) aliuchukua mkuki kutoka mkononi mwake, akaelekea kwa ngamia na kuipiga kwa mkuki.
Imam Hassan (amani iwe juu yake) aliporudi, damu ilionekana kwenye ncha ya mkuki. Muhammad bin Hanafiyya akahuzunika kwa kuwa hakufanikiwa kufanya hivyo, na dalili za masikitiko zikaonekana usoni mwake. Amirul Muuminiin (amani iwe juu yake) akamwambia:
“Usihuzunike, kwa sababu yeye, Hassan, ni mwana wa Mtume, na wewe ni mwana wa Ali.” [3]
Hotuba ya Kihistoria baada ya Shahada ya Baba yake
Fadhila na daraja za Amirul Muuminiin (amani iwe juu yake) zilielezwa katika hotuba ya Imam Hassan Al-Mujtaba (amani iwe juu yake) siku ya shahada ya baba yake kwa namna ifuatayo.
Abu Mikhnaf, mwanahistoria wa Kishia kutoka Kufa, anasimulia:
“Asubuhi ya siku ya shahada ya baba yake, Imam Hassan (amani iwe juu yake), baada ya kumhimidi na kumsifu Mwenyezi Mungu na kumswalia Mtume (rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na Aali zake), alisema:
‘Usiku huu, mtu ameuwawa shahidi ambaye hakuna yeyote aliyemtangulia katika matendo mema, wala hakuna mtu atakayefikia daraja yake.’
Kisha akaongeza:
‘Alikuwa akifanya Jihadi pamoja na Mtume wa Mwenyezi Mungu (rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na Aali zake) na akimlinda kwa nafsi yake. Mtume wa Mwenyezi Mungu alikuwa akimtuma akiwa na bendera yake, huku Jibril akiwa upande wake wa kulia na Mikail upande wake wa kushoto katika medani ya vita. Hakuwa akirudi mpaka Mwenyezi Mungu alete ushindi kupitia mikono yake.
Shahada yake ilitokea katika usiku ambao Isa bin Maryam alipandishwa mbinguni, na Yusha bin Nun, wasii wa Musa, alifariki.
Katika mali ya dunia, aliacha dirham 700 tu ambazo alikusudia kununulia mtumishi kwa ajili ya familia yake.’
Wakati huo, huzuni ilimbana Imam Hassan (amani iwe juu yake) kooni, akalia, na watu pia wakalia pamoja naye. Kisha alisema:
‘Mimi ni mwana wa Mtume (rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na Aali zake), mwana wa mwenye kuita kuelekea kwa Mwenyezi Mungu, na mwana wa familia ambayo Mwenyezi Mungu ameiondolea uchafu. Sisi ndio “Hasana” ambayo Mwenyezi Mungu amewajibisha kwa Umma mapenzi yetu katika Qurani.’
Kisha Imam alisema:
‘Mimi ni mwana wa mtoaji bishara na mwana wa mwonyaji; mwana wa mwenye kuita kuelekea kwa Mwenyezi Mungu, na mwana wa familia ambayo Mwenyezi Mungu ameiondolea uchafu. Sisi ndio “Hasana” ambayo Mwenyezi Mungu amewajibisha kwa Umma mapenzi yetu katika Qurani. Na amesema:
قُلْ لَا أَسْأَلُكُمْ عَلَيْهِ أَجْرًا إِلَّا الْمَوَدَّةَ فِي الْقُرْبَىٰ ۗ وَمَنْ يَقْتَرِفْ حَسَنَةً نَزِدْ لَهُ فِيهَا حُسْنًا ۚ إِنَّ اللَّهَ غَفُورٌ شَكُورٌ
“Sema: Siwaombi ujira wowote juu ya ujumbe huu isipokuwa mapenzi kwa jamaa wa karibu. Na yeyote anayefanya jambo jema, tutamzidishia uzuri ndani yake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kuthamini.” (Aya ya 23 ya Sura ya al-Shura)
Basi “Hasana” ni kutupenda sisi Ahlul Baiti.’” [4]
Utabiri wa Shahada ya Familia ya Utume
Katikati ya machozi ya Amirul Muuminiin (amani iwe juu yake), Mtume wa Mwisho (rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na Aali zake) alifunua mustakabali uliojaa mateso na shahada kwa ajili yake na watoto wake.
Amirul Muuminiin Ali bin Abi Talib (amani iwe juu yake), huku akilia, alikwenda kwa Mtume (rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na Aali zake) na kusema:
“Baba yangu na mama yangu wawe fidia kwako, ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Je, wewe utauawa?”
Mtume (rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na Aali zake) akasema:
“Ndiyo, nitawekewa sumu na kuuwawa shahidi. Na wewe pia utauawa kwa pigo la upanga, na ndevu zako zitapakwa damu ya kichwa chako. Mwanangu Hassan (amani iwe juu yake) atawekewa sumu, na mwanangu Hussein (amani iwe juu yake) atauawa kwa upanga. Atauawa shahidi na mwana wa dhalimu, mwana wa dhalimu; mwana wa najisi, mwana wa najisi; mwana wa mnafiki, mwana wa mnafiki.” [5]
Vyanzo
[1] Al-Irshad, Juzuu ya 2, ukurasa wa 2.
[2] Tafsir Furat al-Kufi, ukurasa wa 79.
[3] Al-Manaqib, Juzuu ya 4, ukurasa wa 21.
[4] Bihar al-Anwar, Juzuu ya 43, ukurasa wa 362.
[5] Kitab Sulaym, Juzuu ya 2, ukurasa wa 834.