Katika siku ya Eid al-Adha, Amirul Muuminina (a.s) alitoa khutba kamili na yenye maana nzito ambayo ina maarifa ya kina ya kidini, hukumu za kisheria na mawaidha ya kimaadili. Khutba hii inaanza kwa sifa na shukrani zisizo na kikomo kwa Mwenyezi Mungu na inasisitiza juu ya ukubwa wa sifa za Mola, udharura wa uchamungu, kupita kwa dunia na majukumu ya waumini kwa Muumba na viumbe.
Kumsifu na Kumtukuza Mwenyezi Mungu Mtukufu Abdulrahman bin Jundab ni shakhsia ambaye katika kunukuu hadithi kutoka kwa baba yake, Jundab bin Abdullah anachukuliwa kuwa ni miongoni mwa wanazuoni wa Tabi’in na miongoni mwa masahaba wa Amirul Muuminina (a.s). Ananukuu kutoka kwa baba yake kwamba: “Amirul Muuminina Ali (a.s) alitoa khutba Siku ya Eid al-Adha. Kisha akaleta takbira na kusema: ‘الله اکبر، الله اکبر، لا اله الا الله، و الله اکبر، الله اکبر، و لله الحمد’, Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu ambaye ametuongoza katika hili; shukrani pia ni Zake, kwa sababu ametujaribu na sifa na shukrani ni za Mwenyezi Mungu pekee kwa yale aliyoturuzuku miongoni mwa wanyama.”
Ukubwa na Sifa za Kiungu Bwana wa Wachamungu aliendelea kusema: “‘الله اکبر’; kwa kiasi cha uzito wa Arshi ya Mwenyezi Mungu, kwa kiasi cha radhi Yake, kwa kiasi cha urefu wa maneno Yake, na kwa idadi ya matone ya mbingu na matone ya bahari. Majina mazuri ni Yake na sifa na shukrani duniani na akhera pia ni Zake pekee; mpaka awe radhi, na hata zaidi ya radhi, kwani Yeye ni Mtukufu na Mkuu. Mwenyezi Mungu ni Mkuu kuliko kila kitu. Yeye ni Mkuu na Mtukufu; Mola Mwenye Nguvu, Mwenye Utukufu, na Mwenye Huruma ambaye rehema Yake imeenea. Yule yule ambaye anakubali toba, anasamehe makosa, na wakati waja Wake bado wana uwezo, kwa sababu ya msamaha, anafuta dhambi kwa kalamu ya msamaha. Hakuna anayekata tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu isipokuwa waliopotea.”
Ushahidi wa Upweke wa Mungu na Utume Amirul Muuminina (a.s) baada ya kumsifu na kumtukuza Mola, alitoa maneno kuhusu upweke wa Mwenyezi Mungu: “Mwenyezi Mungu ni Mkuu sana na kwa ikhlasi nakiri kwamba hakuna mungu apaswaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu Mmoja. Kila asubuhi na kila jioni ninamtakasa na kumuomba. Sifa njema ni za Mwenyezi Mungu pekee; tunamsifu, tunamuomba msaada, na tunamuomba msamaha na uongofu. Ninashuhudia kwamba hakuna mungu apaswaye kuabudiwa isipokuwa Mwenyezi Mungu Mmoja; hana kifani na hana mshirika. Na pia ninashuhudia kwamba Muhammad ni mja Wake na mtume Wake. Yeyote anayemtii Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, bila shaka ameongoka na amepata uokovu mkubwa; na yeyote anayemuasi Mwenyezi Mungu na Nabii Wake, hakika amepatwa na upotovu wa mbali.”
Onyo Kuhusu Kupita kwa Dunia Bwana wa Wachamungu katika mwendelezo wa khutba ya siku ya Eid al-Adha, kuhusu kupita kwa dunia alisema: “Enyi waja wa Mwenyezi Mungu! Ninawausia kumcha Mwenyezi Mungu na kukumbuka mauti mara kwa mara. Jihadharini na dunia ambayo watu kabla yenu hawakufaidika nayo na haitobakia kwa yeyote baada yenu; na jueni kwamba hatima ya wale waliomo ndani yake, ni hatima ile ile ya waliotangulia. Jueni; ni kana kwamba dunia imefikia mwisho na kutangaza kuaga kwake. Mema yake yamebaki kutojulikana, na kwa haraka inawapa kisogo wapenzi wake na kupita; na uharibifu umechanganyika nayo na inawapeleka wale wa karibu nayo kuelekea kwenye mauti.”
Wito wa Kujiandaa kwa Safari ya Milele Amirul Muuminina (a.s) kwa maneno ya kishairi kuhusu kufa kwa dunia hii na nyumba ya kudumu katika mwendelezo wa khutba alisema hivi: “Kile kilichoonekana kuwa kitamu duniani, kinakuwa kichungu; na kile kilichokuwa safi na angavu, kinaelekea kwenye giza. Hakibakii kutoka duniani zaidi ya masalia kama masalia ya maji chini ya chombo au fundo la maji; kiasi kidogo ambacho ikiwa mwenye kiu atakionja, kiu yake haitokatika. Basi enyi waja wa Mwenyezi Mungu, jiandaeni kwa ajili ya kuhama kutoka humo na azimieni kwa dhati kuiacha dunia; kwa sababu hakuna aliye hai anayetamani kubakia milele na hakuna nafsi yoyote isipokuwa imetii amri ya mauti. Jihadharini matamanio yasiwatawale na msifikiri mwisho wa umri na ajali vipo mbali; kwani matokeo yake ni mtakuwa na mioyo migumu. Msidanganyike na matamanio, hila na ahadi za shetani kwani shetani ni adui yenu na ana pupa sana na maangamizi na uharibifu wenu.”
Kumuabudu Mwenyezi Mungu Katika Fursa ya Maisha Amirul Muuminina (a.s) kisha akaeleza: “Enyi waja wa Mwenyezi Mungu, maadamu mpo hai muabuduni Mwenyezi Mungu. Naapa kwa Mwenyezi Mungu ikiwa mtalia kwa uchungu kama ngamia waliochomwa moto na kupoteza watoto wao, na mkalia sana kiasi kwamba sauti yenu ikawa kama ya njiwa wenye huzuni, na mkajitenga na dunia kama watawa wapweke na kupiga kelele na kulia, na kwa ajili ya kuomba ukaribu, kuinua cheo mbele Yake au kuomba msamaha wa dhambi iliyoandikwa na waandishi wa Kiungu na kusajiliwa na malaika, mkajitolea mali na watoto katika njia ya Mwenyezi Mungu, hakika ni kidogo mbele ya thawabu mnayotarajia kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu na mbele ya adhabu Yake mnayoihofia.”
Udhaifu wa Amali za Mwanadamu Mbele ya Neema za Kiungu Amirul Muuminina (a.s) katika kuelezea ukubwa wa neema za Haki Mtukufu alisema: “Naapa kwa Mwenyezi Mungu ikiwa mioyo yenu itayeyuka kabisa kwa kumuogopa Yeye na macho yenu yakatoa machozi ya damu kwa hofu Yake, na kisha mkaishi kulingana na umri wa dunia na kufanya matendo mema kabisa, bado matendo yenu hayataweza kulingana na neema kubwa alizowapeni Mwenyezi Mungu. Nyinyi mnastahili Pepo kwa rehema na fadhila Zake tu. Mwenyezi Mungu atujalie sisi na nyinyi miongoni mwa watu wa uadilifu, toba, na wenye kurejea Kwake.”
Baraka na Utakatifu wa Siku Hii Bwana wa Wachamungu aliichukulia siku ya Eid al-Adha kuwa ni siku kubwa na aliwakumbusha wote adabu na amali zake kwa njia hii: “Jueni kwamba leo ni siku yenye utakatifu mkubwa sana na baraka yake inatarajiwa na katika siku hii msamaha wa dhambi unatarajiwa. Basi mkumbukeni Mwenyezi Mungu sana na kwa toba, kurejea Kwake, unyenyekevu na maombi, jiwekeni katika nafasi ya kupata malipo Yake. Kwani Yeye ndiye anayekubali toba ya waja Wake, anasamehe dhambi, na ni Mwenye huruma na anawapenda waumini.”
Hukumu na Adabu za Kuchinja na Kushukuru Neema Amirul Muuminina (a.s) katika mwendelezo wa hotuba yake alisema: “Ikiwa mtu yeyote miongoni mwenu atachinja, basi achinje kondoo (dume) miongoni mwa kondoo; na kuchinja mbuzi haifanani na hilo. Miongoni mwa dalili za kukamilika kwa mnyama wa kuchinjwa ni macho na masikio yake kuwa salama. Ikiwa macho na masikio yake ni salama, mnyama huyo ni sahihi na kamili; lakini ikiwa pembe yake imevunjika au anavuta mguu wake chini wakati wa kuchinjwa, haitoshi. Mnapofanya ibada ya kuchinja, kuleni katika nyama ya mnyama huyo na mwalishe wengine na wekeni akiba kiasi fulani na mshukuruni Mwenyezi Mungu kwa kuwaruzuku nyama ya wanyama.”
Ushauri Kuhusu Swala, Zaka na Mambo Mengine ya Wajibu Amirul Muuminina (a.s) alisema: “Simamisheni swala, toeni zaka, na fanyeni ibada kwa ukamilifu na uzuri. Huisheni ushahidi wa haki na uadilifu na shikamaneni na kile alichokuwajibishieni Mwenyezi Mungu kwa raghba na utashi. Fanyeni Hija, funga, swala, zaka na alama na dalili za imani alizokuwajibishieni; kwani malipo ya Kiungu ni makubwa na kheri na baraka zake ni nyingi. Aamrisheni mema na mkataze maovu. Msaidieni dhaifu, mnusuruni aliyedhulumiwa, na mzuieni na mkamateni mkono wa dhalimu na yule anayewatia watu katika shaka na wasiwasi.”
Mwenendo Mwema, Ukweli na Jihadi Ilikuwa karibu na mwisho wa khutba ambapo Bwana wa Wachamungu aliwaalika wahudhuriaji kuwa na mwenendo mwema kwa wanawake na akasema: “Muwe na mwenendo mwema kwa wanawake na watumwa wenu. Muwe wakweli katika kuzungumza, rejesheni amana kwa wenyewe, na tekelezeni ahadi na mikataba. Muwe imara katika kutetea haki na uadilifu na toeni kipimo na mizani kamili. Piganeni jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu kama anavyostahiki. Jihadharini maisha ya dunia yasiwadanganye, na shetani mdanganyifu asiwatie katika kiburi na udanganyifu kuhusiana na Mwenyezi Mungu.”
Mwisho wa Khutba kwa Kusoma Qur’ani Amirul Muuminina (a.s) alihitimisha khutba yake muhimu kwa maneno haya: “Bila shaka mawaidha yanayofika zaidi na maneno bora kabisa, ni maneno ya Mwenyezi Mungu.” Kisha Mtukufu huyo akasema “أعوذ بالله من الشیطان الرجیم” (Ninajikinga kwa Mwenyezi Mungu kutokana na Shetani aliyelaaniwa), akasoma Surah Al-Ikhlas, na akaketi kama mtu mwenye haraka; kisha akasimama na kusema: “Sifa na shukrani ni za Mwenyezi Mungu pekee. Tunamsifu, tunamuomba msaada na uongofu, na tunamuomba msamaha na tunamtegemea Yeye.” Kisha katika mwendelezo alitoa khutba fupi, kwa mtindo wa khutba ya swala ya Ijumaa.
Chanzo
Bihar al-Anwar, Juzuu ya 88, Ukurasa 99; Misbah al-Mutahajjid, Ukurasa 363