Most searched:

Utakatifu wa Hazrat Amirul Mu’minin (A.S) chini ya Sababu Imara za Mapokezi na Kiakili

"Ismah" (Utakasifu na kualindwa na madambi au makosa) ni moja ya sifa za Amirul Mu'minin (A.S) ambazo Mtume Mtukufu (S.A.W.W) na hadithi pamoja na riwaya za mutawatir zimesisitiza na kuzithibitisha.

Utakatifu ambao una maana ya kulindwa dhidi ya  kila aina ya makosa, madhambi, na kuteleza katika kauli, vitendo, na tabia, na unahesabiwa kuwa miongoni mwa nguzo muhimu za uongozi (Uimamu) katika Uislamu wa madhehebu ya Shia.

Utakatiifu wa Maimamu na mbele yao akiwa Amirul Mu’minin (A.S) ni miongoni mwa sifa za wazi za familia hii takatifu ambapo sababu nyingi za kiakili na za ki Qurani zimepokelewa kwazo, na utapitia muhimu zaidi kati yazo hapa chini.

Aya ya Tathir

Moja ya maana zilizo wazi kabisa za ismah(utakatifu) ni ile iliyotajwa katika Aya ya “Tathir” ambapo Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: «…إِنَّمَا يُرِيدُ اللَّهُ لِيُذْهِبَ عَنكُمُ الرِّجْسَ أَهْلَ الْبَيْتِ وَيُطَهِّرَكُمْ تَطْهِيرًا» (1) Kwa ajili hiyo, kuondolewa kwa uchafu na kutakasika ni tafsiri iliyo wazi ya maana ya “Ismah”.

Aya ya “Ulil Amri” au “Wilayah”

Miongoni mwa maana nyingine za ismah tunaweza kuashiria Aya ya “Ulil Amri” au “Wilayah”. Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: «يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَطِيعُوا اللَّهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ وَأُولِي الْأَمْرِ مِنكُمْ…» (2)

Utakatifu wa “Ulil Amri” na wajibu wa kuwatii kikamilifu unaenda sambamba na utii kamili kwa Mwenyezi Mungu na Mtume Wake (S.A.W.W), na sharti la utii huu kamili ni kuthibitika kwa ismah. Kwani kutokuwepo kwa ismah kunamaanisha uwezekano wa kutokea dambi, na kukiwa na uwezekano huo utii haujuzu. Pia katika aya tukufu, utii kamili kwa viongozi na kutokuwepo kwa uwezekano wa makosa kwao kunamaanisha kuwa wakati ismah na uwezekano wa makosa haviwezi kukutana sehemu moja, basi jambo hili linamaanisha kuwa mwenye ismah ameepukana kabisa na batili, na kwa njia hii utakatifu wa “Ulil Amri” unathibitika. Kuna aya nyingine nyingi ambazo hakuna nafasi ya kuzitaja hapa, lakini zimeelezwa katika vitabu vya kalaam na itikadi.

Hadithi Muhimu Zinazosisitiza Utakatifu wa Hazrat Amirul Mu’minin (A.S)

Katika sunnah tukufu pia zimetaja katika uwanja huu, na kuna hadithi nyingi za mutawatir ambapo tutaashiria muhimu zaidi kati yazo:

  • Hadithi ya Thaqalayn
  • Hadithi ya “Thaqalayn” ni miongoni mwa hadithi ambazo ni mutawatir kwa madhehebu yote ya Kiislamu. Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W.W) anasema: “Hakika mimi nawaachia mambo mawili mazito na yenye thamani kubwa miongoni mwenu, moja ni kitabu cha Mwenyezi Mungu yaani Qurani, na lingine ni kizazi changu cha Ahlul-Bayt. Fahamuni kwamba wawili hawa ndio makamu wangu baada yangu na hawatatengana kamwe hadi watakaporejea kwangu kwenye Hodhi ya Kawthar.” (3)
  • Kauli ya Mtume (S.A.W.W) kwamba Qurani na kizazi chake ndio makamu wawili baada yake na hawatatengana hadi Siku ya Kiyama, na kwamba Ahlul-Bayt (A.S) ni maasumu na Qurani imethibitisha utakasifu wao ambao hakuna batili itakayowafikia kwa mbele wala kwa nyuma, hii ndiyo maana ya kutotengana. Kizazi ambacho kingefanya makosa au madambi kingetengana na Qurani, na kisingeweza kuwa mshirika au mwandamani wa Qurani.
  • Hadithi ya Ghadir
  • Hadithi ya “Ghadir” nayo ni miongoni mwa hadithi za mutawatir kwa makundi ya Kiislamu. Mtume (S.A.W.W) katika hadithi hii anasema: “Kila niliyokuwa kiongozi wake, basi kuanzia sasa Ali ni kiongozi wake, ewe Mola mpende anayempenda, na mshike kama adui anayemfanya adui.” (4) Na kwamba kiongozi au msimamizi ambaye ni wajibu kutiiwa, utii kamili haufai isipokuwa kwa maasumu pekee.
  • Kauli ya Mtume (S.A.W.W)
  • Kile kinachoonyesha utakatifu wa Maimamu (A.S) na Amirul Mu’minin (A.S) ni kauli ya Mtume (S.A.W.W) isemayo: “Ali yuko na Qurani na Qurani iko na Ali, na hawatatengana kamwe hadi watakapoingia kwenye Hodhi ya Kawthar.” (5)
  • Kile kinachofahamika kutokana na maana ya ismah ni kauli ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W.W) isemayo: “Yeyote anayetaka kuishi na kufa kama nilivyoishi na kufa mimi, na kuishi katika pepo ya Adn ambayo Mola wangu ameiandaa, basi aikubali wilaya ya Ali (A.S) baada yangu, awe rafiki wa wapendwa wake, na afuate Maimamu wanaokuja baada yake, kwani wao ni familia yangu na kizazi cha familia yao kimeumbwa kutokana na udongo wangu, na Mungu amewaruzuku ufahamu na elimu yangu. Ole wao watakaowakataa miongoni mwa umma wangu, ambao rehema yangu itakatika kwao na Mungu hatawapa shufaa yangu.” (7)
  • Kauli ya Imamu al-Sadiq (A.S)
  • Pia Imamu al-Sadiq (A.S) amesema: “Sisi ni maasumu, Mwenyezi Mungu Mtukufu amewaamuru watu tutiiwe na amewakataza kutuasi.” (6)

Sababu za Kiakili za Utakatifu wa Amirul Mu’minin (A.S)

Sababu za kiakili za utakatifu wa Amirul Mu’minin (A.S) ni sawa kabisa na sababu za kiakili zilizotolewa kuhusu utakasifu wa Mtume (S.A.W.W). Kwani Imamu ni mwendelezi wa njia ya Mtume (S.A.W.W), na imethibitishwa kutoka kwake kwamba hazungumzi kwa matamanio ya nafsi; kwani kauli zake si chochote isipokuwa ufunuo ulioshushwa.

Akili (mantiki) ambayo inaeleza kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu hawezi kumtuma mtume asiye maasumu, ndiyo hiyo hiyo inayoeleza kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu hawezi kumweka Imamu asiye maasumu.

Pia, akili inahukumu wajibu wa ismah kwa manabii na Maimamu (A.S), kwa kuzingatia kwamba utii kwao katika kila jambo ni wajibu, na mbele ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kumlazimisha utii mtu asiyemwamini ni uovu na inakwenda kinyume na lengo; kwani Mwenyezi Mungu Mtukufu amewajibisha utii kwa manabii na Maimamu (A.S) katika kila kile wanachosema kwa ajili ya kuwaongoza watu, kuwazindua, na kuwifikisha kwenye ukamilifu wa maisha ya dunia na Akhera.

Bila shaka, mwongoza njia na mwalimu ni lazima awe maasumu kutokana na makosa, ghafla, kusahau, uongo, na maasi ili kuwepo kwa uaminifu kwake na kupokelewa kwa uongofu na amri zake.

Vyanzo

  1. Al-Ahzab, Aya ya 33.
  2. Al-Nisa’i: Aya ya 59.
  3. Al-Amali, Sheikh Al-Saduq: uk 500.
  4. Dala’ilul Imamah: uk 18. Sunan Al-Tirmidhi: Jz 5, uk 633, Hadithi ya 3713.
  5. Al-Bahar: Jz 38, uk 35. Al-Mustadrak: Jz 3, uk 124.
  6. Al-Kafi: Jz 1, uk 369.
  7. Muqtadhabul Athar: uk 16. Hilyatul Awliya: Jz 1, uk 68.

Yaliyomo zaidi

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *