Kwa nini Najaf Ashraf unajulikana kama mji wa misikiti?
Mji wa Najaf Ashraf unatambulika kwa wingi wa misikiti yake. Miongoni mwa misikiti iliyopo katika mji huu mtakatifu, ni upi ulio wa kale zaidi? “Abdul-Hadi Ibrahimi”, mjumbe wa bodi ya usimamizi wa haram takatifu ya Alawi na mtaalamu wa majengo ya kihistoria na kale ya uwanja mtakatifu wa Amirul Muuminin (Amani iwe juu yake), anafafanua hivi:
Najaf Ashraf ni mji mkuu wa Kiislamu na kitovu cha kidini, na misikiti pamoja na husseiniyya zimeenea katika vichochoro vyote vya sehemu ya kale ya mji wa Najaf. Misikiti na husseiniyya hizi zipo katika mipaka ya mitaa minne maarufu ya sehemu ya kale ya mji, ambayo ni: “Mishraq, Buraq, Amarah, na Huwaish”.
Zaidi ya hayo tuliyoyataja, kuna sababu nyingine ya kimantiki ya kuenea kwa misikiti katika mji wa Najaf Ashraf; nayo ni kwamba Marjaa wa taqlidi na wanachuoni mashuhuri hapo zamani walikuwa hawastahimili kuswalisha swala ya jamaa ndani ya uwanja mtakatifu wa Amirul Muuminin (Amani iwe juu yake) au ndani ya haram takatifu, kwani waliona kufanya hivyo ni kuleta kero na kuzuia uhuru wa wafanyaziara.
Kwa mfano, “Sheikh Ja’far Kashif al-Ghita” katika kitabu chake “Kashif al-Ghita”, anabainisha kuwa: “Kusimamisha swala ya jamaa katika uwanja mtakatifu wa Amirul Muuminin (Amani iwe juu yake) ni kupora haki za wafanyaziara!”. Kwa vyovyote vile, hawa walikuwa ni shakhsia, wanachuoni, na mujtahidina waliokuwa na maoni yao maalum. Hali hii ilipelekea Marjaa na wanachuoni wa zamani kuwa na misikiti yao maalum katika mitaa minne ya Najaf ambapo walikuwa wakiswalisha, na wakati huo huo, misikiti hiyo ilikuwa ni vituo vya masomo ya kidini (Hawza) kwa wanachuoni hao.
Misikiti Mashuhuri na ya Kale Zaidi ya Najaf Ashraf
Ikiwa tunataka kuashiria misikiti mashuhuri na ya kale zaidi katika mitaa minne ya mji wa Najaf, lazima tuelekee mtaa wa kale zaidi ambao ni mtaa wa Mishraq.
Msikiti wa kale zaidi katika sehemu yote ya kale ya mji, hususan katika mtaa wa Mishraq – bila kuhesabu misikiti iliyounganishwa na uwanja mtakatifu wa Amirul Muuminin (Amani iwe juu yake) kama vile Msikiti wa Al-Ras, Msikiti wa Imran Shahin, na Msikiti wa Khadhra – ni Msikiti wa Marjaa mkuu “Abu Ja’far al-Tusi”. Abu Ja’far al-Tusi alifariki mnamo mwaka 460 Hijria.
Msikiti wa pili kwa ukale katika mji wa Najaf upo katika mtaa wa Buraq nao ni Msikiti wa “Turihi”. Msikiti huu unanasibishwa na Marjaa mkuu wa zama zake, “Muhaqqiq Sheikh Fakhruddin al-Turihi”, aliyefariki mwaka 1085 Hijria. Baadhi ya watu huunasibisha msikiti huu na zama za nyuma zaidi kwa “Muhaqqiq al-Karaki”, aliyefariki mwaka 940 Hijria.
Katika mtaa wa Amarah, tuna misikiti miwili mashuhuri na ya kale:
- Msikiti wa Jawahiri: Marjaa mkuu “Sheikh Muhammad Hasan”, mtunzi wa kitabu cha “Jawahir”, ndiye aliyeanzisha msikiti huu. Alifariki mwaka 1264 Hijria.
- Msikiti wa Kashif al-Ghita: Marjaa wa taqlidi “Sheikh Musa Al Kashif al-Ghita” alianzisha msikiti huu. Alifariki mwaka 1331 Hijria. Yeye ni mtoto wa Marjaa mkuu Sheikh Ja’far Al Kashif al-Ghita mkubwa.
Mwishoni mwa mtaa wa Huwaish, upo Msikiti wa Hindi. Msikiti huu ulijengwa katika zama za “Allamah Sheikh Hussein Najaf”, aliyefariki mwaka 1251 Hijria. Katika kipindi cha karibuni, Marjaa mkuu “Sayyid Muhsin al-Hakim” alifanya kazi ya kuupanua na kuukarabati msikiti huu.
Msikiti mwingine maarufu ni Msikiti wa “Ansari”, ambao pia unajulikana kama Msikiti wa “Waturuki”. Marjaa mkuu “Sheikh Murtadha al-Ansari” ndiye aliyeanzisha msikiti huu. Alifariki mwaka 1281 Hijria.
Hii ndiyo misikiti muhimu na ya kale zaidi katika sehemu ya kale ya Najaf. Kama tunavyoona, misikiti hii ilianzishwa na Marjaa wa madhehebu ya Shia katika zama hizo.