Most searched:

Kulaumiwa kwa Masahaba kwa Kutokwenda Kwenye Jihad

Amirul Muuminina (amani iwe juu yake) katika hotuba ya 27 ya Nahjul Balagha, kwa kuwakumbusha wito wake wa mara kwa mara wa kwenda kwenye jihadi na kutojali kwa watu, anakosoa utendaji wao mbele ya mashambulizi ya adui.

Amirul Muuminina (amani iwe juu yake) katika hotuba ya 27 ya Nahjul Balagha anasema:

“Jihadi ni mlango miongoni mwa milango ya Peponi ambao Mwenyezi Mungu amewafungulia marafiki Zake maalum. Jihadi ni vazi la uchamungu, ngao madhubuti na kinga ya Mwenyezi Mungu iliyo salama.

Watu wanaogeuzia mgongo jihadi, Mwenyezi Mungu huwavisha vazi la udhalilifu na mabalaa huwashambulia, wanakuwa wanyonge na wadhalilifu, akili na ufahamu wao huharibika, na kwa sababu ya kupoteza jihadi, haki zao hukanyagwa na alama za udhalilifu hudhihirika kwao, nao hunyimwa uadilifu.

Fahamuni kwamba mimi usiku na mchana, kwa siri na dhahiri, niliwaita ninyi kupigana na kundi hili (Muawiya na wafuasi wake) na nikasema piganeni nao kabla hawajapigana nanyi.

Naapa kwa Mwenyezi Mungu, hakuna taifa linaloshambuliwa ndani ya nyumba zake isipokuwa litadhalilika.

Lakini ninyi mlichelewa na mkaacha kutoa msaada mpaka adui akawashambulia mfululizo na akamiliki ardhi yenu.

Sasa sikilizeni, (mmoja wa makamanda wa jeshi la uporaji la Muawiya) kutoka ‘Banu Ghamid’ ameshambulia Anbar (mji wa mpakani) na amemwua mwakilishi na gavana wangu ‘Hassan bin Hassan al-Bakri’ na amewafukuza askari na walinda mipaka wenu kutoka kwenye ardhi hiyo.

Nimefikiwa na habari kwamba mmoja wao ameingia katika nyumba ya mwanamke wa Kiislamu na mwanamke asiye Mwislamu ambaye chini ya ulinzi wa Uislamu maisha na mali yake vilikuwa salama, na amewavua vikuku, bangili, mikufu na masikio kutoka kwenye miili yao…

Wakati ambapo hawakuwa na njia yoyote ya kujilinda isipokuwa kulia na kuomba msaada, wamerejea wakiwa na ngawira nyingi, bila hata mtu mmoja miongoni mwao kujeruhiwa au tone la damu kumwagika kutoka kwao. Ikiwa kwa sababu ya tukio hili Mwislamu atakufa kwa masikitiko, hatalaumiwa na kwa maoni yangu jambo hilo ni la haki na linastahili.

Laiti nisingewona! Ajabu! Ajabu! Naapa kwa Mwenyezi Mungu ukweli huu unaiua mioyo ya wanadamu na huleta huzuni na majonzi, kwamba wao katika njia yao ya ubatili wameungana namna hii, na ninyi katika njia ya haki mmetawanyika na kufarakana namna hii!

Nyuso zenu ziwe mbaya na huzuni iwe pamoja nanyi daima kwa sababu mmekuwa shabaha ya mashambulizi ya adui, wanawashambulia mfululizo na ninyi hamfanyi mashambulizi ya kulipiza kisasi.

Wanapigana nanyi na ninyi hampigani, kwa njia hii Mwenyezi Mungu anaasiwa, na ninyi (kwa vitendo vyenu) mnaridhia jambo hilo.

Kila ninapotoa amri ya kwenda kwa adui wakati wa kiangazi, mnasema tupe muhula kidogo mpaka joto lipungue, na ikiwa nitawapa amri hii wakati wa baridi, mnasema sasa hali ya hewa ni ya baridi kali, acha baridi ipungue!

Visingizio hivi vyote vilikuwa ni kwa ajili ya kukimbia baridi na joto! Nyinyi mnaoogopa na kukimbia baridi na joto, naapa kwa Mwenyezi Mungu mtakimbia zaidi upanga wa adui.

Enyi mnaofanana na wanaume lakini si wanaume! Enyi wenye tabia za kitoto msio na akili! Na enyi maharusi mnaokaa kwenye vyumba vya harusi! (ambao hamfikrii kitu kingine isipokuwa starehe na anasa).

Ni kwa kiasi gani nilitamani nisingewaona wala kuwafahamu, kufahamiana huko ambako hatimaye kumeniacha nikiwa mwenye huzuni daima na mwenye kusononeka. Mwenyezi Mungu awangamize kwani mmeijaza mioyo yangu kwa huzuni na mmejaza kifua changu kwa hasira, na mmeninywesha vikombe vya huzuni na majonzi fundo baada ya fundo. Kwa uasi wenu na kutonisaidia, mmeharibu mipango na mikakati yangu (ya kuliangamiza adui na kujenga jamii bora ya Kiislamu) mpaka Maquraishi wakasema: ‘Mtoto wa Abu Talib ni mtu shujaa lakini hajui mbinu za vita!..’

Mwenyezi Mungu awalipe kheri, je kuna yeyote miongoni mwao mwenye uzoefu zaidi yangu au aliyenitangulia katika nyanja hizi za mapambano?

Mimi niliingia katika uwanja wa mapambano siku hiyo wakati umri wangu ukiwa bado haujafika miaka ishirini, na sasa nimevuka miaka sitini, lakini yule ambaye amri yake haitekelezwi, hana mpango wala mkakati.

(Hata kama mawazo yake yatakuwa ya juu na mipango yake ikiwa makini, hatawahi kufikia matokeo yoyote!)”