Most searched:

Habari za Uvamizi wa Jeshi la Muawiya Kwenye Miji

Katika hotuba ya 25 ya Nahjul Balagha, Amirul Muuminina (amani iwe juu yake) anazungumzia mfarakano na uasi wa wafuasi wake mbele ya haki na utii wa maadui zao kwa ubatili, na anamwomba Mwenyezi Mungu kuwaangamiza na ampe Yeye wasaidizi walio bora zaidi.

Wakati habari za mfululizo zilipomfikia Amirul Muuminina (amani iwe juu yake) kwamba wafuasi wa Muawiya wameiteka baadhi ya miji, na “Ubaidullah bin Abbas” na “Said bin Nimran” magavana wa Imamu huko Yemen walirejea kwa Imamu (amani iwe juu yake) baada ya kushindwa na “Busr bin Abi Artah”.

Amirul Muuminina (amani iwe juu yake) kwa ajili ya kuwakemea wafuasi wake kwa sababu ya kulegalega katika jihadi na kupinga amri zake, alipanda mimbari na kutoa maneno yafuatayo:

“Hakika, kwa njia hii mliyoichukua, hakuna chochote mikononi mwangu isipokuwa Kufa(mji wa iraq), ambayo naweza kuifungua au kuifunga!

Lakini ee Kufa! Ikiwa wewe tu ndiye (rasilimali yangu dhidi ya adui), na tena kwa dhoruba hizi zote, basi uso wako uwe mbaya (na natamani usingekuwepo).

Nimefikiwa na habari kwamba ‘Busr’ ameiteka ‘Yemen’, naapa kwa Mwenyezi Mungu nilijua kwamba hawa watawatawala hivi karibuni, kwa sababu wao wameungana katika kuinusuru batili yao na ninyi mmetawanyika katika njia ya haki, mmesimama kumuasi kiongozi wenu katika njia ya haki lakini wao wanamtii kiongozi wao katika batili yao, wanatekeleza amana kwa kiongozi wao na ninyi mnafanya usaliti, wao wanajishughulisha na mageuzi katika miji yao na ninyi mnafanya uharibifu, ikiwa nitamkabidhi mmoja wenu chombo kama amana, nachelea asije akaiba kamba yake.

Eee Mola wangu! (Kwa kiasi cha kutoa nasaha na maonyo) nimewachosha na kuwasononesha, na wao pia wamenichosha, nimewakinai na wao wamenikinai, nipe watu bora zaidi badala yao, na uweke kiongozi mbaya kuliko mimi juu yao.

Eee Mwenyezi Mungu! Yeyushe mioyo yao kama vile chumvi inavyoyeyuka kwenye maji. Fahamuni kwamba naapa kwa Mwenyezi Mungu, nilitamani badala yenu ningekuwa na wapanda farasi elfu moja kutoka ‘Banu Firas bin Ghanm’ (ili kwa msaada wao niwaweke maadui mahali pao, wao wako kama mshairi alivyosema): Kama lile wingu linalokwenda kasi lenye maji kidogo, wasio na subira na wenye shauku ya kuua adui. Kisha akashuka kwenye mimbari.”