Idara ya Masuala ya Kifikra na Kitamaduni ya Atabatu Tukufu ya Alawiyya imeshiriki kikamilifu katika toleo la 27 la Maonesho ya Kimataifa ya Vitabu ya Baghdad. Ushiriki huo umefanyika kupitia sehemu ya maonyesho yenye upekee kwa ukubwa na eneo lake, pamoja na maudhui ya kitamaduni na maarifa yaliyowasilishwa kwa wageni wa maonesho.
Ammar Mashaallah, Naibu Mkuu wa Idara ya Masuala ya Kifikra na Kitamaduni, alisema katika mahojiano na kituo cha habari: “pavilioni ya Atabatu Tukufu ya Alawiyya ina zaidi ya machapisho 300 ya aina mbalimbali yaliyotolewa na Idara ya Masuala ya Kifikra na Kitamaduni. Machapisho hayo yanahusu nyanja mbalimbali za kifikra, utamaduni na urithi, na yanachangia kutambulisha uzalishaji wa kielimu na maarifa unaowasilishwa na Atabatu Tukufu ya Alawiyya.”
Aliongeza: “Mojawapo ya sehemu maarufu zaidi za banda(pavilioni) au sehemu ya maonyesho hiyo ni Ukuta wa Nahj al-Balagha, wenye eneo la zaidi ya mita za mraba 18. Ukuta huo una mpangilio wa kina unaotambulisha nakala muhimu zaidi za kitabu cha Nahj al-Balagha, pamoja na tafsiri, maelezo na tahakiki zake maarufu zaidi. Sehemu hii, kupitia uwasilishaji wa maarifa, inaangazia hadhi ya kazi hii ya kudumu na juhudi za kielimu na utafiti zilizofanywa juu yake katika historia.”
Alisema: “Banda hilo pia linaonesha mkusanyiko wa magazeti na majarida ya zamani ya Najaf ambayo yamekuwa yakichapishwa katika mji wa Najaf al-Ashraf tangu mwaka 1910.
Miongoni mwa machapisho hayo ni ‘al-Ilm’, ‘al-I’tidal’, ‘al-Hira’ na ‘al-Bayan’, pamoja na machapisho mengine muhimu yanayoakisi sehemu ya historia ya harakati za kitamaduni na vyombo vya habari katika mji huo.”
Aliendelea: “Pia, mkusanyiko wa baadhi ya maandishi muhimu zaidi ya marehemu mwandishi wa khati, Jasim Najafi, umeoneshwa katika banda hilo kutokana na thamani yake ya kisanaa na kiurithi. Aidha, vielelezo vya vitu vya thamani kutoka Hazina ya Alawiyya na makusanyo yake ya nakala za kale zilizoandikwa kwa mkono vimewekwa wazi kwa wageni.”
Qurani inayohusishwa na Amirul Muuminiin (amani iwe juu yake)
Akizungumzia vitu vingine vya thamani vilivyooneshwa katika banda hilo, alisema: “Banda la Atabatu Tukufu ya Alawiyya mwaka huu limetofautishwa kwa kuonesha Qurani Tukufu inayohusishwa na Amirul Muuminiin (amani iwe juu yake).
Qurani hii ni mojawapo ya nakala za kale zilizoandikwa kwa mkono wenye thamani kubwa zaidi katika Hazina ya Alawiyya. Kutokana na thamani yake ya juu sana ya kidini, kihistoria na kiurithi, imepokelewa kwa shauku na kuvutia sana wageni wa Maonesho ya Kimataifa ya Vitabu ya Baghdad.”
Inafaa kutajwa kuwa ushiriki wa idara hii katika maonesho hayo ni fursa muhimu ya kuwasiliana na umma, watafiti na wanaopenda masuala ya utamaduni.
Banda la Atabatu Tukufu ya Alawiyya limepokelewa kwa hamasa kubwa na makundi mbalimbali ya wageni, hususan kutokana na Qurani Tukufu inayohusishwa na Amirul Muuminiin (amani iwe juu yake), machapisho mapya, nakala za kale zilizoandikwa kwa mkono, magazeti na majarida ya zamani ya Najaf, pamoja na Ukuta wa Nahj al-Balagha.






